Mamajusi
“Yuko wapi yeye aliyezaliwa Mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake Mashariki, nasi tumekuja kumsujudia”. (Mt 2:2)
Mamajusi ni Wataalamu wa nyota ,tuwaite “ Wanajimu”.
Mtoto Yesu alipozaliwa mjini Betlehemu kulitokea ishara ya pekee angani. Nyota kubwa yenye kung’ara sana ilionekana angani. Watu wengi waliiona nyota hiyo, miongoni mwao walikuwa mamajusi. Mamajusi ni watu gani? Haw walikuwa wataalamu wa elimu ya nyota. Ni wanasayansi waliopenda kupekua mambo na kutafuta ukweli kupitia elimu ya nyota. Mamajusi walipoiona nyota ya pekee angani, walikumbuka utabiri wa Manabii Mika na Danieli usemao kwamba Masiha atakapozaliwa itatokea nyota ya pekee.
Baada ya kujadiliana, mamajusi watatu waliamua kufanya safari wakiongozwa na nyota hiyo ili kumtafuta Masiha. Majina yao ni Melkiori, Baltazari na Gaspari. Mmoja alitoka Uturuki, wa pili Mongolia na watatu Ethiopia. Watu hawa walitoka kila mmoja katika nchi yake bila kujuana, walikutana njiani wakaanza safari ya kutafuta alikozaliwa Masiha. Bila shaka jamaa, marafiki na jirani zao walijaribu kuwazuia wasichukue uamuzi huo wa hatari, kuifuata hiyo nyota inayowapeleka wasikokujua. Lakini wao walijisemea, tumeona nyota yake twende tukamwabudu. Hatari, uchovu na urefu wa njia havikuwakatisha tama, walidumu mpaka wakafika alikokuwa mtoto Yesu. Walipofika huko Yerusalemu walikwenda kwenye ikulu ya Herode na kumuuliza, “yuko wapi yeye aliyezaliwa Mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake Mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.” Herode anaposikia habari za kuzaliwa kwa Masiha anafadhaika sana na kuhuzunika moyoni. Herode alikuwa kibaraka wa wakoloni wa Kiroma. Kwa hofu ya kunyang’anywa cheo chake aliwauwa watu wote aliowatilia mashaka. Alikuwa mtu katili sana. Alimwua mke wake Mariamu, mama mkwe Alexandra na watoto wake wa kiume watatu. Ndiyo maana Wayahudi walizoea kusema, heri kuwa nguruwe wa Herode kuliko kuwa mtoto wake. Kabla ya kufa kwake aliagiza askari wawakamate watu maarufu na matajiri wa Yerusalemu na kuwatia gerezani. Aliagiza dakika atakapo kufa yeye na hao wote wanyongwe, ili kama watu hawatalia kwa ajili yake, walau watalia kwa ajili ya hao. Je! mfalme wa aina hiyo anaposikia mfalme mwingine amezaliwa atafanya nini? Herode aliwaita wale mamajusi faraghani, akapata kwao hakika ya muda tangu ilipoonekana nyota. Akawapeleka Betlehemu akisema, “shikeni njia, mkaulize sana habari za mtoto, na mkisha kumwona, nileteeni habari ili mimi nami niende nikamsujudie.” Neno sana linaonyesha jinsi Herode alivyo na uchu wa kumwangamiza mtoto Yesu. Lengo lake si kumsujudia mtoto Yesu bali ni kutaka kumwangamiza. Tukumbuke kuwa mafahali wawili hawakai zizi moja. Lakini Yesu hakuja kuwa mfalme wa dunia hii kama Herode alivyofikiri. Ufalme wake ni wa mbinguni, hivyo Herode hakuwa na sababu yeyote ya kutafuta kumwangamiza Yesu. Yesu alikuwa mfalme mpole na mnyenyekevu asiye na makuu. Hali hiyo ilionekana siku alipoingia Yerusalemu akiwa amepanda mwana punda. Hii ni ishara wazi kuwa ufalme wake haukuwa sawa na wafalme wengine wa dunia hii.
Herode anaogopa kupoteza madaraka, akifikiri kwamba Yesu baadae atakuja kumpindua. Anatoa amri ya kuwaua watoto wote wakiume waliozaliwa kipindi cha Yesu, kwa lengo la kumuua mtoto Yesu. Tarehe 28/12 huwa tunaadhimisha sikukuu ya watoto mashahidi, hawa ndiyo waliouwawa na Herode. Herode alikuwa mkatili sana wa kupindukia,inasemekana kwamba alikuwa na historia ya kumwua Shemeji yake kwa kumnyonga (Kaka wa mke wake).Alikuwa ameshamwua pia mke wake na mama mkwe wake (mama wa mke wake). Komesha ya yote unyama wa Herode haukuishia hapo bali inasemekana kwamba aliwahi kuwaua watoto wake watatu. Sasa basi,kumbe kitendo cha kuangamiza watoto hao wachanga wa kiume kwake hakikuwa cha ajabu. Kumbe sasa,ndio maana akatekeleza mauaji ya watoto maelfu na maelfu akimsaka mtoto Yesu.Anawaua kisa,amesikia mtoto Yesu aliyezaliwa ni mfalme. Anawaua akiogopa kupoteza nafasi yake ya ufalme, kwani amesikia mtoto aliyezaliwa ni wa ajabu mwenye ufalme mabegani mwake. Hilo linamtia hofu Herode.
Katika masomo ya siku hiyo tunamsikia nabii Yeremia akituambia hivi “ Bwana asema hivi sauti imesikika Rama, kilio na maombolezo mengi, Raheli akiwalilia watoto wake, asikubali kufarijiwa kwa kuwa hawako”(Yer 31:15-16)
Baada ya Herode kuwaagiza wakachunguze sana habari za mtoto Yesu, hatimaye walifika alipokuwa amezaliwa mtoto Yesu. Walipofika huko walitarajia kumkuta mtoto mfalme katika mji mkuu; lakini wanamkuta Betlehemu mji mdogo. Walitarajia kumkuta katika nyumba ya kifalme, wanamkuta katika nyumba ya kupanga ya mjane Anna. Walitazamia kuwakuta wasujudu wengi, lakini wakawakuta mamae mzazi na Yosefu tu nao ni wageni. Ingawa waliona hayo, lakini wao kwa imani walimtambua mwana wa Mungu. Wakapiga magoti wakamsujudia. Wakafugua mikoba yao wakampa zawadi zao: dhahabu, ubani na manemane.
Dhahabu: ni zawadi yenye thamani ya juu, hutolewa kwa mfalme. Ni ishara ya mapendo na heshima kwa mtawala. Ni ishara kwamba Yesu ni mfalme.
Ubani: hutumika katika ibada, ni alama ya ukuhani wa Yesu. Ubani hutumika katika ibada takatifu ya misa kufukizia altare. Kazi hiyo hufanywa na kuhani, na Yesu ndiye kuhani wetu mkuu. Ni ishara ya kumsujudu na kumwabudu Mugu. Ni ishara ya sala.
Manemane: Ni mafuta mazuri ya kupaka maiti, hutolewa kwa ajili ya maziko ya mwanadamu. Ni ishara kuwa Yesu atajitoa sadaka kwa ajili ya watu, ni ishara ya mateso. Katika Injili ya Mt. 26:12 Yesu anasema “kwa maana kwa kunimwagia mwili wangu marihamu hiyo, ametenda hivyo ili kuniweka tayari kwa maziko yangu.
Kwa kifupi hao mamajusi kwa zawadi zao walikiri kuwa mtoto Yesu ni mfalme, ni Mungu, na ni mwanadamu atakayekufa. Kwa zawadi zao wanatufunza nasi tumpe mtoto Yesu mapendo yetu, kama mfalme wetu tumpe sala zetu kwa kuwa ni Mungu, na tumpe mateso yetu kwa kulipia dhambi zetu.
0 coment�rios: