Sunday, 19 November 2017

Jinsi ya kuomba mchango wa harusi

Kuomba hela kutoka kwa mtu mwingine huwa ni kazi ngumu sana na huwafanya watu wasijiamini. Hebu fikiria umepanda daladala, halafu kondakta anaitisha nauli. Ukiangalia mfukoni una shilingi mia mbili tu, pesa nyingine yote umeisahau nyumbani. Ni hali gani huwa inakupata? Huwa unajipanga vipi kumuomba konda akubali kupokea mia mbili badala ya mia nne ya nauli? Kama huwa unapata wakati mgumu kwa jambo hilo dogo tu, je inakuwaje pale ambapo unataka kuwaomba watu wakuchangie mamilioni kwa ajili ya kuifanikisha harusi yako ambayo kwao haina faida yoyote? Kwanza umshawishi mtu akuchangie mpaka akubali, akishakubali akuahidi kiwango cha fedha ambacho ataweza kukuchangia. Mahali panapokuwa pagumu zaidi ni pale ambapo inabidi uwe unamkumbusha ili atoe fedha aliyoiahidi. Wahenga walisema ‘Ahadi ni deni’, lakini kwa hili inabidi uwe mpole na mvumilivu illi uweze kuupata mchango ulioahidiwa. Ili usiwe na wakati mgumu katika kuomba mchango kwa ajili ya kufanikisha shughuli ya harusi yako, inabidi uzingatie mambo yafuatayo; Usiombe mchango kutoka kwa watu usiowajua Ni kosa kubwa sana kuomba mchango hasa wa harusi kwa watu ambao hufahamiani nao. Kumekuwa na tabia ya watu kuomba marafiki wao wawashawishi marafiki wengine ambao hawawafahamu kuchangia harusi zao. Kumbuka kwamba watu hao huwajui, na hujawahi kuwa na mchango wowote katika Maisha yao. Hivyo siyo vyema kwa vile tu unahitaji mchango wa hausi ndio uombe hata kwa watu usiowafahamu. Vilevile utapata wakati mgumu katika ukusanyaji wa michango kwani kwao ni rahisi kukudanganya. Usipange bajeti ambayo hutoweza kuimudu Harusi nyingi hufanywa kwa gharama kubwa sana. Watu wengi wanaofunga ndoa hupenda kupanga bajeti kubwa ambayo wengine hata hawawezi kuzifikia. Ili kuepusha kuonekana msumbufu au mzigo kwa wengine, hakikisha kuwa unaepuka baadhi ya mambo ili kupunguza gharama za harusi yako. Vile vile usipange bajeti ambayo itakuwa ngumu kufikiwa na kamati yako ya harusi Unapopanga bajeti ya harusi yako, hakikisha kuwa haitokuwa mzigo kwa wale unaowalenga kukuchangia. Hii itakufanya wewe kupata michango kwa wakati na kufanikisha harusi yako. Endapo bajeti yako itakuwa mzigo kwao, basi tegemea kupata michango kwa kuchelewa au kushindwa kuifikia bajeti yako. Toa taarifa mapema iwezekanavyo Hakikihsa unatoa taarifa mapema kuwa unataka kufunga ndoa. Usisubiri mpaka muda uishe ndipo utoe taarifa kuwa unahitaji kuchangiwa. Wape watu taarifa mapema ili nao wapate muda mzuri wa kujiandaa kifedha. Usikuruprke tu kutuma ujumbe katika kundi la WhatsApp kuwa unafunga ndoa mwezi ujao hivyo unahitaji mchango. Kufanya hivi kutakupelekea wewe kuonekana msumbufu na unaweza usipate michango kutoka kwao.

1 comment: