Friday, 4 May 2018

ETI NAIPENDA YANGA? VIPI UKO PEMBENI NA UMEICHA IENDE IKAFE YENYEWE ALGERIA ETI NAIPENDA YANGA? VIPI UKO PEMBENI NA UMEICHA IENDE IKAFE YENYEWE ALGERIA

NA SALEH ALLY MABINGWA wa soka Tanzania, Yanga hakika wanatia huruma hasa kutokana na hali yao ya kimaisha kwa maana ya kifedha. Yanga wameondoka nchini jana kwenda Algeria kuivaa USM Alger katika mechi ya Kombe la Shirikisho. Lakini ukiangalia nyuso za wachezaji wake, zinatia huruma na si vibaya kusema mambo si mazuri. Binafsi ninaona Yanga kwenda kuiwakilisha nchi, wakiwa ni timu kubwa kwa namna walivyokwenda si sahihi hata kidogo na ningependa nikumbushe masuala kadhaa kabla ya kuendelea kusonga. Yanga ilianza kuyumba baada ya kutoa fedha zake zaidi ya Sh milioni 100 kwa ajili ya usajili wa Donald Ngoma ambaye leo hana faida hata kidogo. Acha viongozi waendelee kumpa moyo, lakini hesabu za haraka, kutaka kuridhisha mashabiki, zilichangia wao kuingia katika uamuzi ambao haukuwa sahihi. Sasa mashabiki walifurahi kwa muda kwa kuwa Yanga ililazimika kukopa, lakini mwisho leo wanaumia zaidi kwa kuwa kukopa fedha za mishahara kulipia usajili na kisicho sahihi, kinawaumiza wao leo. Hapa lazima mjifunze kufanya mambo kwa malengo na si kufurahisha watu tu. Pili ninajiuliza, labda ikiwezekana na mashabiki wengine wa Yanga kama wanaweza kutoa jibu, kwamba kama timu iko katika wakati mgumu kama sasa. Vipi hatujaona wanajitokeza wachangiaji? Swali nauliza kwa kuwa ni rahisi sana kuona wachangiaji kama timu inakwenda kucheza mechi dhidi ya watani wake wa jadi, Simba tu! Mechi ya Kombe la Shirikisho, tena dhidi ya timu kama ya Algeria, Yanga wanakwenda utafikiri yatima, nanyi mnakubali, mkiwa mmekaa kando mnasubiri kulaumu tu? Unaipenda Yanga, umefanya nini kusaidia katika hili? Angalau uliwahi hata kutoa ushauri ili kuchangia jambo fulani? Au mko kando Yanga ikifungwa mabao matano, muanze kulalama na kuonyesha mnaipenda timu kwa dhati mnataka kulia au ‘kufa’ kwa kuwa imefanya vibaya? Waungwana jifunzeni, onyesheni uungwana na mbadilike na acheni kabisa kuamini Yanga inapokutana na Simba pekee ndiyo muhimu. Mnafanya hivyo kufurahisha nafsi zenu tu ili muwe na amani mitaani. Si waungwana ambao mnaweza kuwa mashabiki mnaotambua usahihi na ubora wa timu yenu na kile inachoshiriki. Acheni kuipenda Yanga kwa maneno na mbwembwe huku mkiwa mmejaa unafiki wa maneno ambao hauisaidii yenyewe. Nikiachana na mashabiki wa soka, naingia kwenye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambalo ndilo baba wa soka Tanzania. Yanga ni wawakilishi wa Tanzania tena pekee katika michuano ya kimataifa. Wameondoka kama yatima, wasio na ndugu wala mtu wa kuwalilia. Ubaba wa TFF ni upi sasa? Vipi angalau hata TFF isitoe kiasi cha fedha kuikopesha Yanga, ilipe hata mishahara ya miezi miwili na yenyewe ingeweza kutoa taratibu au kukata katika mechi hata zile za Kombe la Shirikisho? TFF haiwezi kushiriki michuano, Yanga ni mwakilishi wao na hata kuingia hatua hiyo tu, shirikisho hilo litafaidika. Sasa vipi haliwezi kujitolea angalau mchango kidogo au mkopo ili kuokoa hali? Kila mechi TFF itapata fedha, lazima Yanga ifanye vizuri zaidi ili iingize fedha zaidi na ikumbuke kama hakuna Yanga na timu nyingine, basi hakuna TFF. Hii si sawa, Yanga imeondoka utafikiri ilipokuwa inaishi kuna wanyama na si wanadamu, maana msaada wake umekuwa ni kutazamwa na waliofanikiwa kuisaidia ni wachache sana. Wanaoipenda wengi si wenye upendo wa dhati, wana upendo wa kinafiki, kizandiki na wazabizabina ndiyo maana wameshindwa kuonyesha wanaweza kuisaidia. Safari ya Yanga inanikumbusha maisha ya uswahilini kwetu katika lile suala la ndugu lawama. Wao wanasubiri kulaumu tu na katika shida hawana msaada wowote. Yanga wamekwenda Algeria lakini mkumbuke, hatujawatendea haki. Wakifungwa, msilielie tena.

0 coment�rios: