Tetesi za usajili ndani ya yanga
Baada ya dirisha dogo la Usajili kufunguliwa jana November 15 vilabu vyote vya ligi kuu Bara vimeingia sokoni ili kutafuta wachezaji wa kuboresha vikosi vyao.
Mabingwa watetezi Young Africans wenye maskani yao katika mtaa wa Jangwani wameingia sokoni kwa ajili ya kusaka washambuliaji watakaoweza kutimiza malengo ya kuwapa mabao kwenye mechi watakazocheza, pamoja na kutaka kufikia malengo ya kutetea taji la Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuona Ngoma na Amissi Tambwe kwa sasa, si wachezaji wa kuwategemea tena kutokana na majeraha ya mara kwa mara yanayowakabili.
Mshambuliaji wa Kagera Sugar, Jafary Kibaya, ndiye mchezaji anayetajwa kuvaa
viatu vya straika wa Yanga, Donald Ngoma, iwapo kama mabingwa hao watetezi wataweka mezani dau la shilingi milioni 35 ukiwa ni mkataba wa miaka miwili.
Baada ya kuwepo kwa tetesi hizo Kibaya alisema ni jambo la kawaida kwa mchezaji kufanya mazungumzo na timu hasa kwenye kipindi hiki cha usajili na jambo kubwa analoliangalia hivi sasa ni nafasi ya kucheza na kiasi cha dau atakalopewa. “Si Yanga tu hata timu nyingine yoyote inayonihitaji nipo tayari kwenda, lakini kwa dau hilo la milioni 35 ambazo nitapewa kabisa kabla ya kuanza kufanya kazi.
Jafary aliongeza kuwa “Kagera Sugar hawana tatizo juu ya kumruhusu kikubwa ni Yanga kufuata taratibu za kunichukua, kwani nina mkataba nao na nimefanya kazi kwa uzuri hivyo sitapenda kuondoka vibaya”.
Wakati huo huo, Meneja wa Kagera Sugar,
Mohamed Hussen, alisema kuwa licha ya
Kibaya kuwa na msaada mkubwa ndani ya
Kagera Sugar, lakini hawaoni tatizo kumpa
baraka zao ili akaangalie maisha mengine
iwapo kama taratibu zitafuatwa.
“Waje tu mezani tuzungumze tukielewana
wala haina tatizo, tunamruhusu Kibaya na
mchezaji mwingine tena kwenda sehemu
atakayohitajika kwa kuwa mpira ni maisha yao, haitapendeza kuwanyima nafasi ya kufanya kazi sehemu wanayohitaji,” alisema.
Kibaya alijiunga Kagera Sugar kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Mtibwa Sugar mwanzoni mwa msimu huu, ambapo Yanga walianza kuvutika na mchezaji huyo baada ya kuwavuruga akina Kelvin Yondani na Andrew Vicent Dante katika mechi ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba.
Iwapo Yanga watafanikiwa kuinasa saini yake, ataweza kusaidiana na Ibrahim Ajib na Obrey Chirwa ambao kwa sasa ndio wanaoibeba safu ya ushambuliaji ndani ya Yanga.
0 coment�rios: