TETESI ZA USAJILI SIMBA NA YANGA NOVEMBER 13-2017
Siku za washambuliaji Laudit Mavugo wa Simba na Donald Ngoma, Amissi Tambwe wa Yanga zimeanza kuhesabika wakati msimu wa dirisha dogo la usajili ukitarajiwa kufunguliwa Novemba 15.
Mastraika hao wa kigeni wa Simba na Yanga wameanza msimu huu vibaya wakiandamwa na majeruha na kupoteza uwezo wao wa kufunga mabao kama ilivyokuwa msimu uliopita.
Mavugo na Ngoma kila mmoja amefunga mabao mawili hadi sasa wakati Tambwe ameshindwa kucheza mechi yoyote kutokana na kuwa majeruhi.
Mwenendo wa wachezaji hao unatoa fursa kwa viongozi wa Yanga kuanza kuangalia washambuliaji wengine wa kuziba mapengo yao wakati huu wakijiandaa na mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Ligi ya Mabingwa Afrika.
Tayari Mavugo amehusishwa na mpango wa kutimkia Gor Mahia ya Kenya inayonolewa na kocha wa zamani wa Simba, Muingereza, Dylan Kerry Januari mwakani.
Habari kutoka Kenya zimedokeza kuwa mazungumzo baina ya mchezaji huyo na uongozi wa Gor Mahia yanakwenda vizuri na uhakika wa kutimka Simba ni mkubwa kutokana na kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi hicho.
Mavugo alijiunga na Simba mwaka 2016, msimu uliopita alifunga mabao saba kwenye ligi na msimu huu mabao mawili tu mpaka sasa.
Wakati Mavugo akitajwa kutimikia Kenya, hali ni mbaya kwa Mrundi Tambwe na Mzimbabwe Ngoma wa Yanga ambao tayari mmoja anahusishwa na mpango wa kutemwa kwenye usajili wa dirisha dogo endapo klabu hiyo itapata mshambuliaji mmoja hatari wa kimataifa na mmoja mzawa ili kuungana na Ibrahim Ajib na Obrey Chirwa.Yanga imeanza kumfuatilia mshambuliaji wa Prisons, Mohammed Rashid ‘Mudi’ aliyefunga mabao matano katika michezo tisa ya Ligi Kuu ili kuziba pengo la Ngoma au Tambwe.
Mbali na washambuliaji wachezaji wengine ambao wako hatari kutupiwa virago na klabu zao kwa upande wa Simba ni beki Shomari Kapombe anayesumbuliwa na majeruhi ya muda mrefu, Yusuph Mlipili, Paul Bundala, Mghana Nicholaus Gyan na Mwinyi Kazimoto. Kiungo wa Simba, Jamal Mnyate anahusishwa kutakiwa na Lipuli ya Iringa na beki wa kushoto Jamal Mwambeleko aliyeweka wazi mapema anataka kusaka timu itakayompa muda mwingi wa kucheza kwa kuwa nafasi yake imedhibitiwa na Mohamed Hussein na Ally Shomary.
Yanga pia inaweza kuwapa mkono wa kwa kheri beki Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Mwinyi Haji, Juma Mahadhi na Matheo Anthony walioshindwa kupata nafasi katika kikosi cha kwanza.
Mchezaji mwingine wa Yanga ambaye hana furaha msimu huu ni kipa Benno Kakolanya aliyesajiliwa msimu uliopita kutoka Prisons ya Mbeya. Kakolanya ameshindwa kuidakia timu hiyo hata mchezo mmoja huku uwepo wa kipa Mcameroon, Youth Rostand ukiwa kikwazo kwake, pia majeruhi ya bega nayo yamechangia kipa kushindwa kuonyesha uwezo wake msimu huu.
‘Ninja’ aliyesajiliwa msimu huu kutoka ya Zanzibar, ameshindwa kufua dafu mbele ya mabeki visiki, Kelvin Yondani, Andrew Vincent ‘Dante’, Nadir Haroub ‘Canavaro’.
Yanga imetangaza kutaka kuongeza beki mwingine wa kimataifa hivyo kuzidi kumpa nafasi finyu Mzanzibar huyo kuendelea kuwa salama ndani ya klabu hiyo.
Wachezaji Juma Mahadhi na Antony wameshindwa kuonyesha uwezo wa kumshawishi kocha George Lwandamina licha ya mara chache kuwapa nafasi, hivyo kuzidi kujiweka katika mazingira magumu ya kuendelea kuwepo ndani ya kikosi hicho.

0 coment�rios: