Friday, 24 November 2017

Simba haikamatiki

SIMBA keshokutwa inatarajiwa kushuka kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, kuvaana na Lipuli ya Iringa, huku Wekundu wa Msimbazi hao wakiwa na matumaini makubwa ya kushinda. Kwa vyoyote itakavyokuwa, Simba watatakiwa kupambana ili kushinda mchezo huo iweze kubaki kileleni mwa Ligi Kuu Tanzania Bara, hasa kwa wakati huu inapokabiliwa na upinzani wa hali ya juu kutoka kwa Azam, Yanga, Mtibwa Sugar na Singida United. Katika msimamo wa ligi hiyo inayodhaminiwa na Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania, Simba inaongoza ikiwa na pointi 22, huku ikifuatiwa na Azam yenye idadi ya pointi kama hizo, lakini Wekundu wa Msimbazi wakiwa kileleni kutokana na kuwa na idadi kubwa ya mabao ya kufunga. Yanga, wanaoshuka kwenye Dimba la Azam Complex kesho kumenyana na Prisons, ipo nafasi ya tatu, ikiwa na pointi 20, huku Mtibwa ikifuatia na pointi zao 17, wakati Singida United wakifuatia baada ya kufikisha pointi 17, sawa na Wakata Miwa hao wa Turiani, Morogoro. Akizungumzia mchezo wao wa Jumapili, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Joseph Omog, alisema hiyo ni zaidi ya mechi kwao, kwani wanahitaji kushinda na kujiongezea pointi. Alisema, wanahitaji pointi tatu kwenye mchezo huo ili kuzidi kuachana mbali zaidi na wapinzani wao, Yanga, kwenye msimamo wa ligi hiyo, kwani wanaona wanataka kuwakaribia. “Hiyo ni zaidi ya mechi kwetu, tunahitaji kupambana ili kupata pointi tatu na kubaki kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo, lakini pia kutaka kutimiza malengo yetu tuliyojiwekea msimu huu,” alisema Omog. Kwa sasa Simba inaendelea na maandalizi yake ya mwisho kuelekea mchezo huo wa raundi ya 11, katika mazoezi yanayofanyika kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini. Msimu huu Simba imeonekana kupania mno kutwaa ubingwa wa Bara, baada ya kuukosa kwa misimu mitano, ikiwakodolea macho watani wao wa jadi, Yanga, wakibeba mwali mara nne, msimu uliopita ikiwa mara tatu mfululizo.

0 coment�rios: